Juma Nature ni miongoni mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya ambao huathiri jamii moja kwa moja kila watoapo albamu au wimbo.Matumizi yake ya lugha,mtindo wake wa kughani au kurap,uhalisia wa kitu anachokiongelea nk ni miongoni mwa mambo ambayo yanamfanya atambe na akubalike zaidi.Hivi karibuni alitoa albamu ambayo ameipa jina la “Tugawane Umasikini”. Baada ya hapo kumekuwa na tafsiri mbalimbali kuhusu “kugawana umasikini”.Bila shaka umeshasikia mtu akikuambia ah…leo ni weekend bwana…ngoja tukagawane umasikini.Starehe mbalimbali zikiwemo ngono,pombe nk zimekuwa ni “kugawana umasikini”.Lakini yeye mwenyewe alikusudia au kumaanisha nini alipozungumzia “Kugawana Umasikini”? Ili kupata jibu kamili nilimtafuta Nature na kufanya naye mahojiano yafuatayo;
UHONDO:Mambo vipi Nature?Umeshamaliza tour ya kuzindua albamu yako?
NATURE: Mambo poa kabisa ndugu yangu.Tour naweza kusema bado inaendelea ingawa baada ya kutembelea mikoa kadhaa hivi sasa nimerejea nyumbani Dar kwa ajili ya mapumziko kidogo na kuangalia masuala ya familia.
UHONDO: Nimekutafuta kwa ajili ya kutaka kujua kitu kimoja; hivi karibuni umetoa albamu ambayo umeiita Tugawane Umasikini. Baada ya kutoka kwa albamu hiyo kumekuwepo na tafsiri mbalimbali kuhusu “kugawana umasikini”.Wengine wanasema kugawana umasikini ni pamoja na kugida maji kwa sana,ngono(zikiwemo zembe) na kwa ujumla kuamua tu kuishi bila kufanya kazi kwa juhudi kwa sababu tayari wengi wetu tu masikini na hivyo hakuna la kufanya.Je, wewe ulimaanisha nini haswa ulipotaka kuzungumzia “kugawana umasikini”?
NATURE: Ahahahaha, labda hapo naweza kusema hiyo ni kazi nzima ya fasihi kwamba kila mtu anaweza kuupokea ujumbe atakavyo au apendavyo na wote wakawa sahihi! Kimsingi nilichomaanisha ni kwamba kutokana na ukweli kwamba nchi yetu na wengi wa wanachi wake bado ni masikini, ni jambo muhimu sana kusaidiana.Pamoja na umasikini tulionao,endapo tutaamua kugawana hicho hicho kidogo tulichonacho basi kwa pamoja tutaweza kuinuana.Baba wa Taifa,Mwalimu Nyerere alipenda sana kutukumbusha kuhusu “Umoja ni Nguvu”.Hapo ndipo alipoongelea sana habari za Ujamaa na Kujitegemea.Leo hii tumesahau misingi ile na ndio maana labda tunaendelea kuwa masikini.Lakini mimi nikiwa nacho kidogo na nikamsaidia mwenzangu,basi kesho si ajabu na yeye akainuka na kumsaidia yule ama yule.Kwa mwendo huo tutafika mahali pazuri zaidi.Isitoshe hatuwezi kuzungumzia utajiri wakati sisi ni masikini.Hivyo ndivyo nilivyoomanisha na ndivyo nilivyokusudia.Wanaopotosha au kujaribu kupindisha maana halisi wanafanya hivyo kwa sababu zao wenyewe zikiwemo kujifariji nk. Lakini kama nilivyotangulia kusema hapo juu,hiyo ni kazi ya fasihi na hivyo siwezi kuwatolea macho au kuwalaumu.
UHONDO: Kama ulivyogusia katika jibu lako hapo juu,watanzania wengi bado ni masikini lakini pia wapo watu ambao ni matajiri wa kutupwa. Una ujumbe gani kwa matajiri hao?
NATURE: Ni kweli kabisa usemalo,wapo matajiri wa kutupwa.Ujumbe wangu kwao ni ule ule labda kwa mtindo tofauti kidogo tu.Badala ya kugawana umasikini wao nitawaambia wagawe utajiri walionao.Wakifanya hivyo nina uhakika wataendelea kuwa matajiri na pia kuinua hali za watu wengine.Umoja ni nguvu.
UHONDO: Kwa mtu ambaye anataka kununua albamu ya Tugawane Umasikini anaweza kuipata wapi?
NATURE: Albamu hivi sasa inapatikana kote mitaani.Lakini kwa uhakika anaweza kuipata pale Mamu Store-Kariakoo.Albamu hii inasambazwa na GMC Wasanii.
No comments:
Post a Comment